1 Samuel 14 (BOKCV)
1 Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. 2 Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600, 3 miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. 4 Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. 5 Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. 6 Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.” 7 Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.” 8 Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. 9 Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. 10 Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba BWANA amewatia mikononi mwetu.” 11 Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” 12 Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.”Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.” 13 Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. 14 Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka. 15 Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu. 16 Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. 17 Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo. 18 Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) 19 Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.” 20 Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. 21 Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. 22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. 23 Hivyo BWANA akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni. 24 Basi watu wa Israeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote ambaye atakula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula. 25 Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwepo na asali ardhini. 26 Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. 27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakawa maangavu. 28 Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.” 29 Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi nilivyopata nguvu mpya nilipoonja asali hii kidogo. 30 Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangalikula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?” 31 Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi mpaka Aiyaloni, walikuwa wamechoka. 32 Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. 33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama yenye damu.”Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” 34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ”Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo. 35 Ndipo Sauli akamjengea BWANA madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu. 36 Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara mpaka mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.”Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.”Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.” 37 Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile. 38 Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. 39 Kwa hakika kama BWANA aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa juu ya mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno. 40 Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.”Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.” 41 Kisha Sauli akamwomba BWANA, Mungu wa Israeli, akisema, “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. 42 Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani. 43 Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.”Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?” 44 Sauli akasema, “Mungu na anishughulikie kwa ukali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.” 45 Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta wokovu huu mkubwa Israeli? Hasha! Hakika kama BWANA aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa. 46 Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao. 47 Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda. 48 Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara. 49 Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali. 50 Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti wa Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. 51 Babaye Sauli yaani, Kishi na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli. 52 Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.