1 Kings 1 (BOKCV)
1 Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo. 2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute kijana mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.” 3 Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. 4 Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura, akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa. 5 Basi Adoniya, ambaye mama yake alikuwa Hagithi, akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia. 6 (Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.) 7 Adoniya akashauriana pamoja na Yoabu mwana wa Seruya na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia. 8 Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, Nathani nabii, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya. 9 Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ngʼombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote, wana wa mfalme na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme, 10 lakini hakumwalika nabii Nathani, Benaya, walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Solomoni. 11 Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Solomoni, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili? 12 Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Solomoni. 13 Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi juu ya kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’ 14 Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.” 15 Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake mahali ambapo Abishagi, Mshunami, alikuwa akimhudumia, naye mfalme alikuwa mzee sana. 16 Bathsheba akasujudu na kupiga magoti mbele ya mfalme.Mfalme akauliza, “Ni nini hiki unachotaka?” 17 Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa BWANA Mungu wako kwamba: ‘Solomoni Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’ 18 Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo. 19 Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Solomoni mtumishi wako. 20 Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi katika kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake. 21 Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Solomoni tutatendewa kama wahalifu.” 22 Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika. 23 Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa ardhi. 24 Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme? 25 Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’ 26 Lakini mimi mtumishi wako, kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni hakutualika. 27 Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?” 28 Ndipo Mfalme Daudi akasema, “Mwite Bathsheba, aingie ndani.” Hivyo akaingia mbele ya mfalme na kusimama mbele yake. 29 Ndipo mfalme akaapa: “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka kila taabu, 30 hakika nitatekeleza leo kile nilichokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli: Mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu, naye ataketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu.” 31 Kisha Bathsheba akasujudu akipiga magoti mbele ya mfalme uso wake ukigusa ardhi akasema, “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!” 32 Mfalme Daudi akasema, “Mwite kuhani Sadoki ndani, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Walipofika mbele ya mfalme, 33 akawaambia: “Wachukueni watumishi wa bwana wenu pamoja nanyi na mkamkalishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu mwenyewe mkamteremshe hadi Gihoni. 34 Huko kuhani Sadoki na nabii Nathani wamtie mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Pigeni tarumbeta na mpaze sauti, ‘Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!’ 35 Kisha mtapanda pamoja naye, atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na kutawala badala yangu. Nimemweka awe mtawala juu ya Israeli na Yuda.” 36 Benaya mwana wa Yehoyada akamjibu mfalme, “Amen! BWANA, Mungu wa bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo. 37 Kama vile BWANA alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe na Solomoni kukifanya kiti chake cha utawala kuwa kikuu kuliko kile cha bwana wangu Mfalme Daudi!” 38 Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakampandisha Solomoni juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. 39 Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka kwenye hema takatifu na kumtia Solomoni mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!” 40 Na watu wote wakakwea wakimfuata, wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti. 41 Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele yote haya katika mji?” 42 Hata alipokuwa anasema, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu mstahiki kama wewe ni lazima alete habari njema.” 43 Yonathani akajibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Solomoni kuwa mfalme. 44 Mfalme amemtuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, 45 nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme huko Gihoni. Kuanzia hapo wameendelea kushangilia na sauti zimeenea pote mjini. Hizo ndizo kelele unazosikia. 46 Zaidi ya hayo, Solomoni ameketi juu ya kiti chake cha ufalme. 47 Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumtakia heri bwana wetu Mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Solomoni kuwa mashuhuri kuliko lako na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake 48 na kusema, ‘Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi juu ya kiti changu cha ufalme leo hii.’ ” 49 Katika hili, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa mshtuko wa hofu na kutawanyika. 50 Lakini Adoniya kwa kumwogopa Solomoni, akaenda na kushika pembe za madhabahu. 51 Kisha Solomoni akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Solomoni na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Solomoni na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ” 52 Solomoni akajibu, “Kama akijionyesha kuwa mtu mstahiki, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi, lakini kama uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” 53 Ndipo Mfalme Solomoni akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Solomoni, naye Solomoni akamwambia, “Nenda nyumbani kwako.”