1 Samuel 15 (BOKCV)
1 Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye ambaye BWANA alinituma nikutie mafuta uwe mfalme juu ya watu wake Israeli, basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa BWANA. 2 Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri. 3 Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ngʼombe na kondoo, ngamia na punda.’ ” 4 Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu 200,000 pamoja na watu 10,000 kutoka Yuda. 5 Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni. 6 Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki. 7 Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila mpaka Shuri, hadi mashariki ya Misri. 8 Akamchukua Agagi, mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga. 9 Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi na kondoo na ngʼombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa. 10 Kisha neno la BWANA likamjia Samweli kusema: 11 “Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia BWANA usiku ule wote. 12 Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli amekwenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.” 13 Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “BWANA akubariki! Nimetimiza yale BWANA aliniagiza.” 14 Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ngʼombe ninaousikia ni kitu gani?” 15 Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ngʼombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.” 16 Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile BWANA aliloniambia usiku huu.”Sauli akajibu, “Niambie.” 17 Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli? BWANA alikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli. 18 Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’ 19 Kwa nini hukumtii BWANA? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa BWANA?” 20 Sauli akasema, “Lakini nilimtii BWANA. Nilikamilisha ile kazi ambayo BWANA alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao. 21 Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwa BWANA Mungu wako huko Gilgali.” 22 Lakini Samweli akajibu:“Je, BWANA anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihukama vile kuitii sauti ya BWANA?Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,nako kusikia ni borakuliko mafuta ya kondoo dume. 23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.Kwa sababu umelikataa neno la BWANA,naye amekukataa wewekuendelea kuwa mfalme.” 24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya BWANA na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka. 25 Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu BWANA.” 26 Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la BWANA, naye BWANA amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!” 27 Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akangʼangʼania pindo la joho lake, nalo likararuka. 28 Samweli akamwambia, “BWANA ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe. 29 Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.” 30 Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu BWANA Mungu wako.” 31 Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu BWANA. 32 Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.”Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.” 33 Lakini Samweli akasema,“Kama upanga wako ulivyofanya wanawakekufiwa na watoto wao,ndivyo mama yako atakavyokuwahana mtoto miongoni mwa wanawake.”Naye Samweli akamuua Agagi mbele za BWANA huko Gilgali. 34 Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli. 35 Hadi siku Samweli alipofariki hakwenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwombolezea. Naye BWANA alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.