Jeremiah 32 (BOKCV)
1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza. 2 Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzunguka mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda. 3 Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka. 4 Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe. 5 Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi mpaka nitakapomshughulikia, asema BWANA. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ” 6 Yeremia akasema, “Neno la BWANA lilinijia kusema: 7 Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulinunua.’ 8 “Kisha, kama BWANA alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’“Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la BWANA. 9 Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba za fedha. 10 Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani. 11 Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri, 12 nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi. 13 “Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao: 14 ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu. 15 Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’ 16 “Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwomba BWANA: 17 “Ee BWANA Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. 18 Wewe huonyesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni BWANA Mwenye Nguvu Zote, 19 makusudi yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kama yanavyostahili matendo yake. 20 Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na umeyaendeleza mpaka leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo mpaka leo. 21 Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa matisho makuu. 22 Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali. 23 Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao. 24 “Tazama jinsi tumezungukwa na jeshi ili kuuteka mji huu. Kwa sababu ya upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo ambao wanaushambulia. Ulilosema limetokea kama vile unavyoona sasa. 25 Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee BWANA Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha, na jambo hilo lishuhudiwe.’ ” 26 Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: 27 “Mimi ndimi BWANA, Mungu wa wote wenye mwili. Je, kuna jambo lolote lililo gumu nisiloliweza? 28 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo BWANA: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa Wakaldayo, na mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ambaye atauteka. 29 Wakaldayo ambao wanaushambulia mji huu watakuja na kuuchoma moto na kuuteketeza, pamoja na nyumba ambamo watu wamenikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba katika mapaa na kumimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine. 30 “Watu wa Israeli na wa Yuda hawakufanya kitu kingine ila uovu mbele zangu tangu ujana wao. Naam, watu wa Israeli hawakufanya kitu kingine ila kunikasirisha kwa kazi ambazo mikono yao imetengeneza, asema BWANA. 31 Tangu siku ulipojengwa hadi sasa, mji huu umenikasirisha na kunighadhibisha kiasi kwamba ni lazima niuondoe machoni pangu. 32 Watu wa Israeli na wa Yuda wamenikasirisha kwa uovu wote waliofanya: wao, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu. 33 Walinigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao. Ingawa niliwafundisha tena na tena, hawakupenda kusikiliza wala kuitikia adhabu. 34 Waliweka miungu yao ya kuchukiza sana katika nyumba iitwayo kwa Jina langu na kuinajisi. 35 Wakajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu kwa ajili ya Baali katika Bonde la Ben-Hinomu, ambapo walitoa wana wao na binti zao kafara kwa Moleki, ingawa kamwe sikuamuru, wala halikuingia akilini mwangu, kwamba watafanya chukizo kama hilo na kumfanya Yuda atende dhambi. 36 “Mnasema kuhusu mji huu, ‘Kwa upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli,’ lakini hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli asemalo: 37 Hakika nitawakusanya kutoka nchi zote nilizowafukuzia katika hasira yangu kali na ghadhabu yangu kuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwaruhusu waishi kwa salama. 38 Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. 39 Nitawapa moyo mmoja na kutenda pamoja, ili kwamba waniche daima kwa mema yao wenyewe na kwa mema ya watoto wao baada yao. 40 Nitafanya nao agano la milele: Kamwe sitaacha kuwatendea mema, nami nitawavuvia kunicha mimi, ili kamwe wasigeukie mbali nami. 41 Nitafurahia kuwatendea mema, na kwa hakika nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na roho yangu yote. 42 “Hili ndilo asemalo BWANA: Kama nilivyoleta maafa haya makubwa kwa watu hawa, ndivyo nitakavyowapa mafanikio niliyowaahidi. 43 Kwa mara nyingine tena mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo mlisema, ‘Imekuwa ukiwa, isiyofaa, isiyo na watu wala wanyama, kwa sababu imetiwa mikononi mwa Wakaldayo.’ 44 Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, na hati zitatiwa sahihi, zitatiwa muhuri na kushuhudiwa katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, katika miji ya Yuda na katika miji ya nchi ya vilima, sehemu za magharibi katika miji ya tambarare na katika Negebu, kwa sababu nitarudisha tena mafanikio yao, asema BWANA.”