John 8 (BOKCV)
1 Lakini Yesu akaenda katika Mlima wa Mizeituni. 2 Alfajiri na mapema Yesu akaja tena Hekaluni, watu wote wakakusanyika, akakaa akaanza kuwafundisha. 3 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote. 4 Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. 5 Katika sheria, Mose alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa wewe wasemaje?” 6 Walimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki.Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake. 7 Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” 8 Akainama tena na kuandika ardhini. 9 Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10 Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?” 11 Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.”Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”] 12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” 13 Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.” 14 Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. 15 Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma. 17 Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti. 18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.” 19 Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?”Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.” 20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia. 21 Yesu akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi ninyi hamwezi kuja.” 22 Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?” 23 Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini, mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 24 Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.” 25 Wakamuuliza, “Wewe ni nani?”Naye Yesu akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo. 26 Nina mambo mengi ya kusema juu yenu na mengi ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kweli, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.” 27 Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia juu ya Baba yake wa Mbinguni. 28 Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha. 29 Yeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’ ” 30 Wengi waliomsikia Yesu akisema maneno haya wakamwamini. 31 Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. 32 Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.” 33 Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” 34 Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. 36 Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. 37 Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. 38 Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.” 39 Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.”Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu. 40 Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Abrahamu hakufanya jambo la namna hii. 41 Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.”Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.” 42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. 44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. 45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! 46 Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? 47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.” 48 Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?” 49 Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau. 50 Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi. 51 Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu hataona mauti milele.” 52 Ndipo Wayahudi wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu. Ikiwa Abrahamu alikufa na vivyo hivyo manabii, nawe unasema ‘Mtu akitii neno langu hatakufa milele.’ 53 Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa na manabii ambao nao pia walikufa? Hivi wewe unajifanya kuwa nani?” 54 Yesu akawajibu, “Kama nikijitukuza utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi. 55 Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake. 56 Baba yenu Abrahamu alishangilia kwamba angaliiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.” 57 Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, wewe wasema umemwona Abrahamu?” 58 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Abrahamu hajakuwako, ‘Mimi niko.’ ” 59 Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.