Joshua 19 (BOKCV)
1 Kura ya pili ikaangukia kabila la Simeoni, ukoo kwa ukoo. Urithi wao ulikuwa ndani ya eneo la Yuda. 2 Ulijumuisha:Beer-Sheba (au Sheba), Molada, 3 Hasar-Shuali, Bala, Esemu, 4 Eltoladi, Bethuli, Horma, 5 Siklagi, Beth-Markabothi, Hasar-Susa, 6 Beth-Lebaothi na Sharuheni; hii ilikuwa miji kumi na mitatu pamoja na vijiji vyake. 7 Pia Aini, Rimoni, Etheri, na Ashani; hii ilikuwa miji minne na vijiji vyake, 8 pamoja na vijiji vyote vinavyoizunguka miji hii mpaka Baalath-Beeri (ambayo ndiyo Rama iliyo katika Negebu).Huu ulikuwa ni urithi wa kabila la Simeoni ukoo kwa ukoo. 9 Urithi wa Wasimeoni ulitolewa kutoka fungu la Yuda, kwa kuwa fungu la Yuda lilikuwa kubwa kuliko walivyohitaji. Hivyo kabila la Simeoni lilipewa urithi wao ndani ya eneo la Yuda. 10 Kura ya tatu ikaangukia kabila la Zabuloni, ukoo kwa ukoo:Mpaka wa urithi wao uliendelea hadi Saridi. 11 Kuelekea upande wa magharibi ukafika Marala, ukagusa Dabeshethi, na kuendelea mpaka kwenye bonde karibu na Yokneamu. 12 Ukageuka mashariki, kuanzia Saridi kuelekea mawio ya jua hadi kwenye nchi ya Kisiloth-Tabori, na kwenda hadi Daberathi, kupanda Yafia. 13 Kisha ukaendelea mashariki hadi Gath-Heferi na kufika Eth-Kasini, ukatokea Rimoni na kugeuka kuelekea Nea. 14 Huko mpaka ukazungukia upande wa kaskazini hadi Hanathoni na kuishia katika Bonde la Ifta-Eli. 15 Miji mingine iliyojumuishwa ni Katathi, Nahalali, Shimroni, Idala na Bethlehemu. Kulikuwa na miji kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. 16 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa ndio urithi wa Zabuloni, ukoo kwa ukoo. 17 Kura ya nne ikamwangukia Isakari, ukoo kwa ukoo. 18 Eneo lao lilijumuisha:Yezreeli, Kesulothi, Shunemu, 19 Hafaraimu, Shioni, Anaharathi, 20 Rabithi, Kishioni, Ebesi, 21 Remethi, En-Ganimu, En-Hada na Beth-Pasesi. 22 Mpaka ule ukagusa Tabori, Shahasuma na Beth-Shemeshi, na ukaishia kwenye Yordani. Ilikuwa miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake. 23 Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Isakari, ukoo kwa ukoo. 24 Kura ya tano ikaangukia kabila la Asheri, ukoo kwa ukoo. 25 Eneo lao lilijumuisha:Helkathi, Hali, Beteni, Akishafu, 26 Alameleki, Amadi na Mishali. Upande wa magharibi mpaka uligusa Karmeli na Shihor-Libnathi. 27 Tena ukageuka mashariki kuelekea Beth-Dagoni, ukagusa Zabuloni na Bonde la Ifta-Eli, ukaenda upande wa kaskazini hadi Beth-Emeki na Neyeli, ukipitia Kabul upande wa kushoto. 28 Ukaendelea hadi Abdoni, Rehobu, Hamoni na Kana, na kufika Sidoni Kuu. 29 Mpaka huo ukageukia nyuma kuelekea Rama na kwenda hadi kwenye mji wenye ngome wa Tiro, ukageuka kuelekea Hosa na kutokeza baharini katika eneo la Akzibu, 30 Uma, Afeki na Rehobu. Ilikuwepo miji ishirini na miwili, pamoja na vijiji vyake. 31 Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa ndio urithi wa kabila la Asheri, ukoo kwa ukoo. 32 Kura ya sita ikaangukia kabila la Naftali, ukoo kwa ukoo: 33 Mpaka wao uliendelea kutoka Helefi na kwenye mti mkubwa ulio katika Saananimu, ukipitia Adami-Nekebu na Yabineeli hadi Lakumu, na kuishia katika Mto Yordani. 34 Mpaka ukaendelea magharibi kupitia Aznoth-Tabori na kutokea Hukoki. Ukagusa Zabuloni upande wa kusini, Asheri upande wa magharibi, na Yordani upande wa mashariki. 35 Miji yenye ngome ilikuwa Sidimu, Seri, Hamathi, Rakathi, Kinerethi, 36 Adama, Rama, Hazori, 37 Kedeshi, Edrei, na En-Hasori, 38 Ironi, Migdal-Eli, Horemu, Beth-Anathi na Beth-Shemeshi. Kulikuwa na miji kumi na tisa na vijiji vyake. 39 Miji hiyo pamoja na vijiji vyake ndio iliyokuwa urithi wa kabila la Naftali, ukoo kwa ukoo. 40 Kura ya saba ikaangukia kabila la Dani, ukoo kwa ukoo. 41 Eneo la urithi wao lilijumuisha:Sora, Eshtaoli, Iri-Shemeshi, 42 Shaalabini, Aiyaloni, Ithla, 43 Eloni, Timna, Ekroni, 44 Elteke, Gibethoni, Baalathi, 45 Yehudi, Bene-Beraki, Gath-Rimoni, 46 Me-Yarkoni na Rakoni, pamoja na eneo linalotazamana na Yafa. 47 (Lakini Wadani walipata shida kulimiliki eneo lao; kwa hiyo walipanda kuishambulia Leshemu, wakaitwaa, wakawaua watu wake kwa upanga na kuukalia. Walikaa Leshemu na kuuita Dani kufuatana na jina la baba yao.) 48 Miji hii na vijiji vyake ndio iliyokuwa urithi wa kabila la Dani, ukoo kwa ukoo. 49 Walipomaliza kugawanya nchi katika migawo kulingana na sehemu zao zilizowaangukia, Waisraeli wakampa Yoshua mwana wa Nuni urithi katikati yao, 50 kama vile BWANA alivyokuwa ameamuru. Walimpa mji alioutaka, ambao ni Timnath-Sera ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu. Naye akajenga mji, akakaa huko. 51 Haya ndiyo maeneo ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa koo za kabila za Israeli waliyoyagawanya kwa kura huko Shilo mbele za BWANA penye ingilio la Hema la Kukutania. Hivyo wakamaliza kuigawanya nchi.