Ezekiel 41 (BOKCV)
1 Kisha yule mtu akanileta katika sehemu ya nje ya patakatifu, naye akaipima miimo; upana wake ulikuwa dhiraa sita kila upande. 2 Ingilio lilikuwa la upana wa dhiraa kumi na kuta zilizojitokeza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa tano. Pia akapima sehemu ya nje ya patakatifu, nayo ilikuwa na urefu wa dhiraa arobaini na upana wa dhiraa ishirini. 3 Kisha akaingia sehemu takatifu ndani ya Hekalu na kupima miimo ya ingilio, kila mmoja ulikuwa na upana wa dhiraa mbili. Ingilio lilikuwa na upana wa dhiraa sita, na kuta zilizotokeza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa saba. 4 Naye akapima urefu wa sehemu takatifu ndani, nao ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini hadi mwisho wa sehemu ya nje ya sehemu takatifu. Akaniambia, “Hapa ndipo Patakatifu pa Patakatifu.” 5 Kisha akapima ukuta wa Hekalu, nao ulikuwa na unene wa dhiraa sita, na kila chumba cha pembeni kuzunguka Hekalu kilikuwa na upana wa dhiraa nne. 6 Vyumba vya pembeni vilikuwa na ghorofa tatu, kimoja juu ya kingine, kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Kulikuwa na boriti katika ukuta wote wa Hekalu ili kuimarisha vyumba vya pembeni, kwa hiyo boriti hizo hazikushikamanishwa kwenye ukuta wa Hekalu. 7 Vyumba vya pembeni vilivyozunguka Hekalu vilizidi kupanuka kulingana na sakafu zilivyokwenda juu. Ujenzi uliozunguka Hekalu ulijengwa kukwea juu, kwa hiyo vyumba vilipanuka kwa kadiri ya kila kimoja kilivyokwenda juu. Ngazi za kupandia zilianzia sakafu ya chini hadi sakafu ya juu kabisa kwa kupitia sakafu ya kati. 8 Nikaona pia kuwa Hekalu lilikuwa na kitako kilichoinuliwa pande zote, huu ulikuwa ndio msingi wa vile vyumba vya pembeni ambao ulikuwa na urefu wa ule ufito mmoja wa kupimia, yaani, dhiraa ndefu sita. 9 Ukuta wa nje wa vyumba vya pembeni ulikuwa na unene wa dhiraa tano. Eneo la wazi katikati ya vyumba vya pembeni vya Hekalu 10 na vyumba vya makuhani lilikuwa na upana wa dhiraa ishirini kuzunguka Hekalu pande zote. 11 Kulikuwa na maingilio kwenye vyumba vya pembeni kutokea eneo lililo wazi, moja upande wa kaskazini na lingine upande wa kusini, nao msingi uliounganisha lile eneo la wazi ulikuwa na upana wa dhiraa tano ukilizunguka lote. 12 Jengo lililoelekeana na ua wa Hekalu upande wa magharibi lilikuwa na upana wa dhiraa sabini. Ukuta wa jengo hilo ulikuwa na unene wa dhiraa tano, kulizunguka lote, urefu ulikuwa wa dhiraa tisini. 13 Kisha akapima Hekalu, lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na ua wa Hekalu na jengo pamoja na kuta zake vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja pia. 14 Upana wa ua wa Hekalu upande wa mashariki, pamoja na upande wa mbele wa Hekalu ulikuwa dhiraa mia moja. 15 Kisha akapima urefu wa jengo linaloelekeana na ua upande wa nyuma wa Hekalu, pamoja na vyumba vyake kila upande, ilikuwa dhiraa mia moja.Sehemu takatifu ya nje, sehemu takatifu ya ndani, pamoja na baraza inayoelekeana na ukumbi, 16 pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta mpaka kwenye madirisha na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao. 17 Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la sehemu takatifu ya ndani, na katika kuta zilizozunguka sehemu takatifu ya ndani na sehemu takatifu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa, 18 kulinakshiwa makerubi na miti ya mitende. Miti ya mitende ilikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili: 19 upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote. 20 Kuanzia sakafu mpaka eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na miti ya mitende pamoja na kwenye ukuta wa nje wa patakatifu. 21 Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulikuwa unafanana na huo mwingine. 22 Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza ambayo iko mbele za BWANA.” 23 Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili. 24 Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango. 25 Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na miti ya mitende kama yale yaliyonakshiwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioningʼinia mbele ya baraza kwa nje. 26 Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa miti ya mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.