Exodus 38 (BOKCV)
1 Akatengeneza madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa mbao za mti wa mshita, kimo chake dhiraa tatu; nayo ilikuwa mraba, urefu wake dhiraa tano, na upana wa dhiraa tano 2 Akatengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu zikawa zimeungana, akafunika madhabahu kwa shaba. 3 Akatengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama na vyombo vya kuchukulia moto. 4 Akatengeneza wavu wa shaba chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu. 5 Akasubu pete za shaba za kushikilia ile mipiko kwa ajili ya zile pembe nne za huo wavu wa shaba. 6 Akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuifunika kwa shaba. 7 Akaiingiza ile mipiko kwenye zile pete, ili iwe pande mbili za madhabahu kwa ajili ya kuibeba. Akaitengeneza madhabahu yenye uvungu ndani yake akitumia mbao. 8 Akatengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kutoka kwa vioo vya shaba vilivyotolewa na wanawake waliohudumu pale ingilio la Hema la Kukutania. 9 Kisha akatengeneza ua. Upande wa kusini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, na ulikuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri, 10 pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo. 11 Upande wa kaskazini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo. 12 Upande wa mwisho wa magharibi ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini na ulikuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo. 13 Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, pia ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini. 14 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu. 15 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mwingine wa ingilio la ua, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu. 16 Mapazia yote yaliyozunguka ua yalikuwa ya kitani iliyosokotwa vizuri. 17 Vitako vya nguzo vilikuwa vya shaba. Kulabu na tepe juu ya nguzo zilikuwa za fedha, na ncha zake zilifunikwa kwa fedha. Kwa hiyo nguzo zote za ua zilikuwa na tepe za fedha. 18 Pazia la ingilio la ua lilikuwa la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini kama zile za kwenye ua, na kimo chake kilikuwa dhiraa tano, 19 likiwa na nguzo nne na vitako vinne vya shaba. Kulabu zake na tepe zake zilikuwa za fedha, na ncha zake zilikuwa zimefunikwa kwa fedha. 20 Vigingi vyote vya maskani na vya ua ulioizunguka vilikuwa vya shaba. 21 Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani, maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Mose, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni. 22 (Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu BWANA alichomwamuru Mose, 23 akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.) 24 Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta 29 na shekeli 730, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. 25 Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli 1,775, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. 26 Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume 603,550. 27 Talanta hizo 100 za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na pazia: vitako mia moja kwa talanta mia, yaani, talanta moja kwa kila kitako. 28 Akatumia zile shekeli hizo 1,775 kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo na kutengeneza vitanzi vyake. 29 Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta 70 na shekeli 2,400. 30 Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote, 31 vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya Maskani pamoja na ule ua uliozunguka.