Exodus 35 (BOKCV)
1 Mose akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo BWANA amewaamuru ninyi mfanye: 2 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya kupumzika kwa BWANA. Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe. 3 Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.” 4 Mose akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo BWANA aliloamuru: 5 Toeni sadaka kwa BWANA kutoka mali mliyo nayo. Kila mmoja aliye na moyo wa kupenda atamletea BWANA sadaka ya dhahabu, fedha na shaba; 6 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi; singa za mbuzi; 7 ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita; 8 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri; 9 vito vya shohamu, na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani. 10 “Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu BWANA alichoamuru: 11 Maskani pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako; 12 Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia; 13 meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonyesho; 14 kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga; 15 madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya maskani; 16 madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na tako lake; 17 pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, pazia la ingilio la kwenye ua; 18 vigingi vya hema kwa ajili ya maskani pamoja na ua na kamba zake; 19 mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.” 20 Ndipo jumuiya yote ya Waisraeli ilipoondoka mbele ya Mose, 21 na kila mmoja aliyependa na ambaye moyo wake ulimsukuma alikuja na kuleta sadaka kwa BWANA, kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, kwa ajili ya huduma yake yote na kwa ajili ya mavazi matakatifu. 22 Wote waliokuwa na utayari, wanaume kwa wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kama sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA. 23 Kila mmoja aliyekuwa na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi, au singa za mbuzi, ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, au ngozi za pomboo, wakavileta. 24 Wale waliotoa sadaka ya fedha au shaba wakavileta kama sadaka kwa BWANA, na kila aliyekuwa na mti wa mshita kwa ajili ya kazi yoyote ile akauleta. 25 Kila mwanamke aliyekuwa na ujuzi alisokota kwa mikono yake na alileta kile alichosokota, iwe ni nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi. 26 Wanawake wote waliopenda na waliokuwa na ujuzi wakasokota singa za mbuzi. 27 Viongozi wakaleta vito vya shohamu pamoja na vito vingine vya thamani kwa ajili ya kuweka kwenye kisibau na kwenye kifuko cha kifuani. 28 Wakaleta pia vikolezi na mafuta ya zeituni kwa ajili ya mwanga, kwa ajili ya mafuta ya upako na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri. 29 Waisraeli wote waume kwa wake waliokuwa wanapenda wakaleta mbele za BWANA kwa hiari yao wenyewe sadaka kwa ajili ya kazi yote ya BWANA aliyokuwa amewaagiza kuifanya kupitia kwa Mose. 30 Kisha Mose akawaambia Waisraeli, “Tazameni, BWANA amemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 31 naye amemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, na uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 32 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 33 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi wa kupendeza. 34 Tena amempa yeye pamoja na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine. 35 Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zifanywazo na mafundi, na wenye kubuni michoro, pia na watarizi kwa rangi za buluu, zambarau, nyekundu na kitani safi, na wafumaji: wote wakiwa mafundi na wabunifu hodari.