Genesis 34 (BOKCV)
1 Basi Dina, binti wa Yakobo aliyezaliwa na Lea, akatoka nje kuwatembelea wanawake wa nchi ile. 2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile alipomwona, akamchukua na kumnajisi. 3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza. 4 Shekemu akamwambia baba yake Hamori, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.” 5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake, kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo mpaka waliporudi nyumbani. 6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo. 7 Basi wana wa Yakobo walikuwa wamerudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotokea. Walikuwa wamejawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti wa Yakobo, kitu ambacho hakingepasa kufanyika. 8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. 9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. 10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.” 11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. 12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.” 13 Kwa sababu ndugu yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na baba yake Hamori. 14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili, hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hakutahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu. 15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote. 16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi. 17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua ndugu yetu na kuondoka.” 18 Pendekezo lao likawa jema kwa Hamori na Shekemu mwanawe. 19 Kijana mdogo, ambaye alikuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo. 20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walikwenda kwenye lango la mji kuzungumza na wenzao wa mjini. 21 Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu. 22 Lakini watu hao watakuwa tayari kukubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao. 23 Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.” 24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa. 25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume. 26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka. 27 Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa. 28 Wakachukua kondoo na mbuzi, ngʼombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani. 29 Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao. 30 Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmeleta taabu kwangu kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu waishio katika nchi hii. Sisi ni wachache, kama wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.” 31 Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”