Luke 1 (BOKCV)
1 Kwa kuwa watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotukia katikati yetu, 2 kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale waliokuwa mashahidi walioyaona na watumishi wa Bwana, 3 mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo, 4 ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa. 5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni. 6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. 7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana. 8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, 9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. 10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba. 11 Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria. 12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. 13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. 16 Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. 17 Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.” 18 Zekaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” 19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. 20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.” 21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. 22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono. 23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake. 24 Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano. 25 Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.” 26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. 28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” 29 Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” 30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. 31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. 33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” 34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” 38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha. 39 Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi. 40 Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti. 41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, 42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.” 46 Naye Maria akasema:“Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, 47 nayo roho yangu inamfurahiaMungu Mwokozi wangu, 48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhiliunyonge wa mtumishi wake.Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa, 49 kwa maana yeye Mwenye Nguvuamenitendea mambo ya ajabu:jina lake ni takatifu. 50 Rehema zake huwaendea wale wamchao,kutoka kizazi hadi kizazi. 51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake;amewatawanya wale wenye kiburindani ya mioyo yao. 52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi,lakini amewainua wanyenyekevu. 53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri,bali matajiri amewafukuza mikono mitupu. 54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli,kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu 55 Abrahamu na uzao wake milele,kama alivyowaahidi baba zetu.” 56 Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake. 57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume. 58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye. 59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake. 60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.” 61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.” 62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. 63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” 64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote. 66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. 67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema: 68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa. 69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovukatika nyumba ya Daudi mtumishi wake, 70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabiiwake watakatifu tangu zamani, 71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao: 72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetuna kukumbuka Agano lake takatifu, 73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu: 74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,tupate kumtumikia yeye pasipo hofu 75 katika utakatifu na haki mbele zake,siku zetu zote. 76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;kwa kuwa utamtangulia Bwanana kuandaa njia kwa ajili yake, 77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovuutakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao, 78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,nuru itokayo juu itatuzukia 79 ili kuwaangazia wale waishio gizanina katika uvuli wa mauti,kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.” 80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.