Mark 6 (BOKCV)
1 Yesu akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake. 2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake! 3 Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini. 4 Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani kwake.” 5 Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.Kisha Yesu akawa anakwenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha. 7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu. 8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.” 10 Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.” 12 Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi. 13 Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya. 14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” 15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.” 16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!” 17 Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” 19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza, 20 kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza. 21 Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta. 22 Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.” 23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” 24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.” 25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” 26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. 27 Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani, 28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini. 30 Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.” 32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi. 35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana. 36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.” 37 Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200 ili tuwape watu hawa wale?” 38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” 39 Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40 nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. 41 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42 Watu wote wakala, wakashiba. 43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000. 45 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. 46 Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba. 47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” 51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu. 53 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54 Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Yesu. 55 Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.