Jeremiah 50 (BOKCV)
1 Hili ndilo neno alilosema BWANA kupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo: 2 “Tangazeni na mhubiri katikati ya mataifa,twekeni bendera na mkahubiri;msiache kitu chochote, bali semeni,‘Babeli utatekwa;Beli ataaibishwa,Merodaki atajazwa na hofu kuu.Sanamu zake zitaaibishwana vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’ 3 Taifa kutoka kaskazini litamshambulia,na kuifanya nchi yake ukiwa.Hakuna hata mmoja atakayeishi ndani yake,watu na wanyama wataikimbia. 4 “Katika siku hizo, wakati huo,”asema BWANA,“watu wa Israeli pamoja na watu wa Yudawataenda wakilia ili kumtafuta BWANA Mungu wao. 5 Wataiuliza njia iendayo Sayunina kuelekeza nyuso zao huko.Watakuja na kuambatana na BWANAkatika agano la mileleambalo halitasahaulika. 6 “Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea;wachungaji wao wamewapotoshana kuwasababisha kuzururajuu ya milima.Walitangatanga juu ya mlima na kilima,na kusahau mahali pao wenyewe pa kupumzikia. 7 Yeyote aliyewakuta aliwala;adui zao walisema, ‘Sisi hatuna hatia,kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi ya BWANA, malisho yao halisi, BWANA, aliye tumaini la baba zao.’ 8 “Kimbieni kutoka Babeli;ondokeni katika nchi ya Wakaldayotena kuweni kama mbuzi wale waongozao kundi. 9 Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babelimuungano wa mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini.Watashika nafasi zao dhidi yake,naye kutokea kaskazini atatekwa.Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari,ambao hawawezi kurudi mikono mitupu. 10 Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara;wote wamtekao nyara watapata za kutosha,”asema BWANA. 11 “Kwa sababu hushangilia na kufurahi,wewe utekaye urithi wangu,kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka,na kulia kama farasi dume, 12 mama yako ataaibika mno,yeye aliyekuzaa atatahayari.Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote,atakuwa nyika, nchi kame na jangwa. 13 Kwa sababu ya hasira ya BWANA hatakaliwa na mtu,lakini ataachwa ukiwa kabisa.Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihakikwa sababu ya majeraha yake yote. 14 “Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli,enyi nyote mvutao upinde.Mpigeni! Msibakize mshale wowote,kwa kuwa ametenda dhambi dhidi ya BWANA. 15 Piga kelele dhidi yake kila upande!Anajisalimisha, minara yake inaanguka,kuta zake zimebomoka.Kwa kuwa hiki ni kisasi cha BWANA,mlipizeni kisasi;mtendeeni kama alivyowatendea wengine. 16 Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna.Kwa sababu ya upanga wa mdhalimukila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe,kila mmoja na akimbiliekwenye nchi yake mwenyewe. 17 “Israeli ni kundi lililotawanyikaambalo simba wamelifukuzia mbali.Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,wa mwisho kuponda mifupa yakealikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.” 18 Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo:“Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yakekama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru. 19 Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewenaye atalisha huko Karmeli na Bashani;njaa yake itashibishwajuu ya vilima vya Efraimu na Gileadi. 20 Katika siku hizo, wakati huo,”asema BWANA,“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,lakini halitakuwepo,kwa ajili ya dhambi za Yuda,lakini haitapatikana hata moja,kwa kuwa nitawasamehemabaki nitakaowaacha. 21 “Shambulieni nchi ya Merathaimuna wale waishio huko Pekodi.Wafuatieni, wauenina kuwaangamiza kabisa,”asema BWANA.“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru. 22 Kelele ya vita iko ndani ya nchi,kelele ya maangamizi makuu! 23 Tazama jinsi nyundo ya dunia yoteilivyovunjika na kuharibika!Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwamiongoni mwa mataifa! 24 Nimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli,nawe ukakamatwa kabla haujafahamu;ulipatikana na ukakamatwakwa sababu ulimpinga BWANA. 25 BWANA amefungua ghala lake la silahana kuzitoa silaha za ghadhabu yake,kwa kuwa BWANA Mwenyezi Mwenye Nguvu Zoteanayo kazi ya kufanyakatika nchi ya Wakaldayo. 26 Njooni dhidi yake kutoka mbali.Zifungueni ghala zake za nafaka;mlundikeni kama lundo la nafaka.Mwangamizeni kabisana msimwachie mabaki yoyote. 27 Waueni mafahali wake wachanga wote;waacheni washuke machinjoni!Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,wakati wao wa kuadhibiwa. 28 Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeliwakitangaza katika Sayunijinsi BWANA, Mungu wetu alivyolipiza kisasi,kisasi kwa ajili ya Hekalu lake. 29 “Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,wote wale wavutao upinde.Pigeni kambi kumzunguka kabisa,asitoroke mtu yeyote.Mlipizeni kwa matendo yake;mtendeeni kama alivyotenda.Kwa kuwa alimdharau BWANA,yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 30 Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;askari wake wote watanyamazishwa siku ile,”asema BWANA. 31 “Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,”asema Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,“kwa kuwa siku yako imewadia,yaani, wakati wako wa kuadhibiwa. 32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,wala hakuna yeyote atakayemuinua;nitawasha moto katika miji yake,utakaowateketeza wote wanaomzunguka.” 33 Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote:“Watu wa Israeli wameonewa,nao watu wa Yuda pia.Wote waliowateka wamewashikilia sana,wanakataa kuwaachia waende. 34 Lakini Mkombozi wao ana nguvu; BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.Atatetea kwa nguvu shauri laoili alete raha katika nchi yao,lakini ataleta msukosukokwa wale waishio Babeli. 35 “Upanga dhidi ya Wakaldayo!”asema BWANA,“dhidi ya wale waishio Babelina dhidi ya maafisa wake na watu wenye busara! 36 Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo!Watakuwa wapumbavu.Upanga dhidi ya mashujaa wake!Watajazwa na hofu kuu 37 Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vitapamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake!Wao watakuwa kama wanawake.Upanga dhidi ya hazina zake!Hizo zitatekwa nyara. 38 Ukame juu ya maji yake!Nayo yatakauka.Kwa kuwa ni nchi ya sanamu,wao wanaenda wazimu kwa ajili ya sanamu. 39 “Kwa hiyo, viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo,nao bundi watakaa humo.Kamwe haitakaliwa tenawala watu hawataishi humo kutoka kizazi hadi kizazi. 40 Kama vile Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomorapamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”asema BWANA,“vivyo hivyo hakuna mtu yeyoteatakayeishi humo.Naam, hakuna mtu yeyoteatakayekaa humo. 41 “Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini;taifa kubwa na wafalme wengiwanaamshwa kutoka miisho ya dunia. 42 Wamejifunga pinde na mikuki;ni wakatili na wasio na huruma.Wanatoa sauti kama bahari inayongurumawanapoendesha farasi zao;wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vitaili kukushambulia, ee Binti Babeli. 43 Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu,nayo mikono yake imelegea.Uchungu umemshika,maumivu kama ya mwanamke katika utungu wa kuzaa. 44 Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordanikuja kwenye nchi ya malisho mengi,ndivyo nitamfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula.Ni nani aliye mteule,nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?Ni nani aliye kama mimi,na ni nani awezaye kunipinga?Tena ni mchungaji yupiawezaye kusimama kinyume nami?” 45 Kwa hiyo, sikia kile BWANA alichokipanga dhidi ya Babeli,kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo:Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali.Yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao. 46 Kwa sauti ya kutekwa kwa Babeli, dunia itatetemeka;kilio chake kitasikika pote miongoni mwa mataifa.